data:post.body NAMNA 4 YA KUFADIKA NA KARANTINI. ~ SIRI ZA AFYA BORA...

Recent Posts

NAMNA 4 YA KUFADIKA NA KARANTINI.



David Duncan Kipeta


Dunia imevamiwa na adui ambaye kwa kiasi kikubwa sisi kama wakazi wa dunia yetu hatukuwa tumejiandaa kubabiliana naye. Ametumavia na kutupiga na kisha kutusambaratisha kila mtu na kwake, watu wamejifungia na hawathubutu kutoka nje huku baadhi ya mataifa watu wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi za kila siku lakini wakiwa na hofu na wenye tahadhari kubwa wakiogopa kukutana na huyu adui mkubwa na mbaya mwenye kusababisha watu kupata homa kali, mafua makali, vichwa kuuma na mbaya zaidi wanapata homa kali sana ya mapafu yenye kusababisha mfumo wa upumuaji kuwa wa shida. Hali inakuwa mbaya sana kwa ndugu zetu wenye magonjwa ya muda mrefu na yenye kuathiri sana mfumo wa kinga wa mwili. Magonjwa kama kisukari, kifua kikuu, shinikizo la damu, virusi vya ukimwi/Ukimwi yanaongeza hatari ya madhara yatokanayo na adui yetu huyu. Huyu adui anaitwa CORONA VIRUS INFECTION DISEASE OF 2019 (COVID19).


COVID19 ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona ambayo huambukizwa haswa kwa kushika au kugusa majimaji yanayotoka kwa mtu mwenye maambukizi hayo. Ugonjwa huu ulianzia na kugunduliwa huko nchini China katika mji wa Wuhan mwishoni mwa mwaka 2019 na ulianza kushamili kuanzia mwezi wa Disemba mwaka huo. Ugonjwa huu uligunduliwa na Daktari Lee Chen ambaye alifarika hapo baadaye kwa maambukizi ya COVID19. Njia zinazosababisha kuenea kwa ugonjwa huu ni kuvuta hewa yenye viini vya virusi vya corona, kushikana mikono, kugusa nguo za muathirika wa virusi vya corona, kushika vitu vilivyoshikwa na mtu mwenye virusi vya corona.

NAMNA YA KUJIKINGA NA COVID19
Nchi nyingi zimeweka namna ya kupunguza maambukizi ya ugonjwa huu kwa kuzuia mikusanyiko ya wananchi, kusisitiza kanuni bora za afya hasa kwa kunawa mikono na sabuni au vitakasa mikono(hand sanitizer), kuvaa barakoa (face masks) na zuio la kuchangamana (social distancing). Lakini jambo kubwa na muhimu linalofanywa kwa watu wanaohisiwa kuwa na maambukizi ni kuzuiwa kuchangamana na watu wasiohisiwa kuwa kuwa na maambukizi. Njia hii inatambulika kama karantini.

Karantini ni kitendo cha kuzuia au kujizuia kutokuchagamana na watu wengine ikiwa mtu fulani amehisiwa au anahisi kwamba amepata maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwa tiba au chanjo ya ugonjwa huo haijapatikana. Wikipedia kamusi inaeleza kuwa “karantini inamaanisha kuzuia miendo ya watu ambao wanaweza kuathiriwa na ugonjwa wa kuambukiza ilhali ugonjwa kwao haukuweza kuthibitishwa bado… karantini hutumiwa pia kama mgonjwa anazuiliwa kukutana na watu wengine ili kuzuia uenezaji wa ugonjwa hatari. Karantini inaweza kutumika kwa wanadamu, lakini pia kwa wanyama wa aina mbalimbali, na wote kama sehemu ya udhibiti wa mpakani na ndani ya nchi”.
Ingawa karantini hufanana zaidi na kutengwa, maneno haya mawili yanamaana tofauti. Kutengwa ni kitendo cha kumuweka mtu aliyethibitika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kuambukiza mbali na watu wengine ili kuzuia maambukizi yasienee.
 Kikawaida karantini huwekwa kwa muda wa siku arobaini
(40) Japokuwa inaweza kuwa muda wa siku kadhaa kuanzia saba (7) na kuendelea.


NAMNA YA KUFAIDIKA NA KARANTINI
 Katazo la kutembea na kuchanganyika na watu lina faida sana kwa nchi ili kuzuia kuenea kwa maambukizi na hivyo kufanya mamlaka za afya kuwa na mzigo mdogo katika kushughulikia watu wachache wenye maambukizi na wenye dalili za maambukizi. Karantini husaidia katika kufuatilia mienendo ya watu na kufuatilia visa vya maambukizi kwa urahisi na umakini mkubwa. Hii husaidia pia katika kupunguza matumizi ya vifaa tiba ambavyo vingetumika kwa watu wengi ambao wangeambukizwa.
 Pamoja na faida zote hizo kwa nchi au jamii fulani pia mtu mmoja mmpoja anaweza kufaidika sana kwa uwepo wa karantini. Faida hizo zaweza kuwa za kiafya, kiuchumi, kimahusiano au kijamii. Katika makala hii tutangalia namna unavyoweza kufaidika na karantini.

Sura ya Kwanza

AFYA

Karantini inaweza kuwa na faida sana kwa mtu binafsi ikiwa ataliangalia jambo hili kama nafasi ya pekee ya kujenga afya njema ya mwili wake. Kabla ya karantini watu wengi hawajali afya zao kama inavyotakiwa kwani watu hawalali kwa muda wa kutosha, kula vizuri na kwa kutulia, kupata muda mwingi wa kujisomea na hata kufanya mazoezi na kadharika lakini wakati wa karantini unaweza kumsaidia mtu kujenga afya bora ya mwili wake ikiwa ataliangalia jambo hili katika mtazamo chanya. Afya bora wakati huu wa karantini inaweza kujengwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

Kupata muda wa kutosha wa kupumzika.
Kitabibu mtu mzima anatakiwa kupata muda usiopungua masaa nane (8) ili kupumzika. Muda huu unatakiwa kutumiwa hasa kwa kulala. Watu wengi wanakosa muda wa kutosha ili mkulala wakati wa usiku. Kulala masaa nane wakati wa usiku ni muhimu sana ili kujenga afya bora ya akili,mfumo wa uzazi, mfumo wa kinga, mfumo wa utoaji taka mwili na hata mmeng’enyo bora wa chakula.
 Kukosa muda wa kutosha wa kulala husababisha kutengenezwa kwa kemikali kama cortisol ambayo huharibu sana afya ya akili na hata viungo vingi vya mwili ikiwemo moyo, maini, figo na hata viungo vya uzazi kutokana na uwingi wa kemikali hii katika damu. Ubongo huanza kukosa kupumzika na hivyo huweza pia kumfanya mtu akose usingizi na baada ya muda mrefu mtu anaweza kupata magonjwa ya akili ikiwemo hasira za karibu zisizo na sababu, kiharusi, msongo wa mawazo na hata sonona.

Mfumo wa kinga huathiriwa sana ukosefu wa usingizi kwa sababu ya uwepo mkubwa wa kemikali ya cortisol ambayo huathiri na hta kuua seli lindaji (white blood cells) zinatotumika kulinda mwili dhidi ya magonjwa. Hivyo ili kuwa na mfumo wa kinga ulio boira na imara ni muhimu sasna kupata muda mwingi wa kulala.
Kukosa muda wa kulala wa kutosha huathiri sana mfumo wa uzazi. Na hii ni moja kati ya sababu kubwa sana za upungufu wa nguvu za kiume, kukosa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake na wanaume na hata kukosa kufurahia tendo la ndoa. Tafiti mbali mbali zimefanyika na kuonyesha kwamba ukosefu wa usingizi hupunguza uzalishaji wa homoni ya kiume iitwayo testosterone ambayo ndio hufanya kazi ya kuongeza msukumo au hamu ya kufanya tendo la ndoa. Homoni hii ipo kwa uwingi sana kwa wanaume na kwa kiwango kidogo kwa wanawake. Homoni hii pia hujulikana sana kama sexual driver yaani kiamshi au kisukumo cha kufanya tendo la ndoa. Hivyo ukitaka kuwa na afya njema ya mfumo wa uzazi na kufanya vizuri na kufurahia tendo la ndoa, usingizi ni muhimu sana. Kipindi hiki cha karantini ni kipindi cha wewe kuirudisha na kujenga heshima katika kitanda chako na mwezi wako lakini tu itafanyika hivyo ukipata muda mwingi wa kupumzika kila siku.
Hizo pamoja na athari zingine kama mmeng’enyo mbaya wa chakula, kuharibika kwa mfumo wa utoaji takamwili ambao huathiri sana figo na maini zinasababishwa kukosa muda wa kutosha wa kulala hivyo katika kipindi hiki cha karantini ni muhimu sana kupata muda wa kutosha kupumzika kwa kulala usingizi si chini ya masaa nane (8) kwa mtu mzima na mtoto kuanzia masaa kumi (10). Usingizi ni Afya.

Kula Vizuri
 Chakula ni afya. Ili kuwa na afya bora ni muhimu kuzifuata kanuni za afya ikiwepo kula chakula bora. Kabla ya karantini watu wengi hula vyakula visivyo vizuri na visivyo na virutubisho vya kutosha ili kujenga afya bora. Vyakula maarufum kama fast foods au junk food mfano wa chips zinazouzwa, vinapoliwa mara kwa mara na kwa muda mrefu hudhoofisha afya kwa kuzorotesha mifumo mbali ya mwili wa binadamu. Vyakula vya kujenga mwili, vyakula vya kulinda mwili na vya kuupa mwili nguvu hutakiwa kutumiwa kwa uwingi kwa kipindi hiki cha karantini.
 Vyakula vya kujenga mwili kama maziwa, mayai, samaki, nyama, maharage na mboga za majani pamoja na vile vya kulinda mwili kama maini, samaki, mboga za majani, matunda ni muhimu na vinahitajika kwa kiwango kikubwa sana kwa kipindi hiki cha karantini bila kusahau vyakula vya kuupa mwili nguvu ili kuendelea na shughuli nyine muhimu za nyumbani.

Kufanya Mazoezi
Katika kuhakikisha umuhimu wa mazoezi katika kipindi hiki cha karantini, hivi karibuni Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Mseveni alionekana katika picha na mitandao ya kijamii akiwa nyumbani kwake akifanya mazoezi mbalimbali ya viungo ikiwemo push up. Alifanya hivi ili kuhimiza umma kuhusu umuhimu wa mazoezi ya viungo huku wakiendelea kubakia ndani katika makazi yao na si kufanyia mazoezi nje kwenye umati wa watu kama gym na hata katika viwanja vya mazoezi au kukimbia nje. Jambo hili la kufanya mazoezi nje au mbali na makazi huweza kuongea hatari ya kupata maambukizi ya vizuri vya COVID19. Uwepo wa katazo la kutoka nje na kuchangamana na watu kwa sababu ya kuogopa kuenea kwa COVID19 sio sababu na isiwe sababu ya kuacha kufanya mazoezi ya viungo. Unaweza kufanya mazoezi ya kutosha hata katika chumba chako cha kulala. Hivyo naomba nikusihi kuendelea kufanya mazoezi ya viungo kila siku na katika makazi yako. Mwanasaikolojia na mwandishi wa kitabu cha The Barbarians at the PTA anashauri kuwa “Endelea kufanya mazoezi na rafiki zako. Ikiwa unapata uvivu kufanya mazoezi peke yako, unaweza kupanga ratiba na rafiki zako ili kufanya mazoezi kama yoga na mengineyo kwa njia ya video katika muda mmoja”[1]
Kumbuka: Afya yako ni mtaji wako na mtaji huu hujengwa na mkukuzwa kwa kula chakula bora, kulala vizuri na kufanya mazoezi.
 Nakutakia heri katika kuendelea kujenga mtaji wako.


Sura ya Pili

UCHUMI

Kipindi inapotanghazwa karantini ni kipindi ambacho hofu ya kudorora kwa uchumi huwa kubwa sana. Uchumi hudorora kwa kwa watu binafsi, makampuni na hivyo hata kwa taifa. Hofu hii huwa kubwa kutokana na ukweli kwamba watu hupunguza kwenda kazini na wengine huacha kabisa. Kutokana na kutofanyika kwa shughuli za kiuchumi, watu huweza kuwa na hali mbaya kiuchumi hasa wale wasio na ajira za kudumu au waliojiajiri wenyewe. Lakini kwa shghuli zisizohamishika au zinazohitaji uwepo wa mtu husika mahali pa kazi hali yaweza kuwa mbaya zaidi tofauti na zile zinazoweza kuhamishika.

Pamoja na ukweli huu wa mabadiliko ya kiuchumi bado tunaweza kuwa na tumaini la kufanya kazi kama kawaida lakini kwa mfumo mwingine. Natamani uangalie mfano wa Mwandishi wa habari na mchekeshaji wa kipindi cha televisheni cha The Daily Show cha nchini Marekani Ndugu Trevor Noah. Yeye ameendelea na shughuli zake za kutoa habari na kuchekesha huku akisalia katika makazi yake. Muongozaji na mchekeshaji wa kipindi cha The Hellen Show, Hellen amekua akiendelea na kazi zake kama kawaida lakini akiwa katika makazi yake. Lakini pia mmiliki wa kampuni ya Zoom Video Communications inayoongoza kwa utoaji wa huduma ya mikutano kwa njia ya video (Video teleconferencing) ndugu Eric Yuan amekuwa akiendelea kufanya kazi na mikutano yake kwa njia ya video. Njia hii ni njia maarufu ikiwa kuna vizingiti kama hivi ya karantini au kutokana na umbali wa wahusika. Pia kulingana na aina za kazi hasa za kiofisi, watu hufanya kazi zao majumbani katika kompyuta na kuzituma katika ofisi zao. Hivyo kufanya shughuli zao kama kawaida.

Kipindi hiki cha karantini kikitumiwa vizuri kinaweza kuwa cha faida kubwa kwa mtu mmoja mmoja. Kuna mambo mengi ambayo mtu anaweza kuyafanya ambayop yakaleta faida kubwa kwa uchumi binafsi na kwa nchi nzima kwani watu wengi hukaa nyumbani. Mambo haya ni kama yafuatayo:

Kuongeza ujuzi wa kiuchumi
Kipindi hiki cha karantini kinaweza kutumiwa katika kuongeza ujuzi katika fani mbali mabali za maisha kwani watu wengi wanakuwa huru na hawajabanwa na majukumu mengi. Ujuzi huu huweza kuongezwa kwa kusoma vitabu au kutembelea tovuti mbalimbali zenye kufundisha maudhui ya kazi fulani na hata namna bora ya kufanya uwekezaji.

Biashara za mitandaoni na uwekezaji (Online marketing and investments).
Hizi ni aiana za biashara ambazo hufanyika kwa njia ya mtandao na mara zote haihitaji wahusika kukutana kwani mnunuzi huagiza mahitaji yake na kuyalipia kwa njia ya mtandao na kisha mahitaji yake hayo hutumwa kwa njia ya posta au kuletewa hadi katika makazi yake na mtu mwingine ambaye hufanya kazi ya kubeba mizigo.
Uwekezaji wa mitandaoni ni njia nzuri pia kwa kipindi hiki kwani huweza kufanya uchumi wako baada ya kipindi cha karantini ya COVID19 kuwa mzuri. Uwekezaji huu huweza kutumia mitandao kama Expert option

Tahadhari: Ni muhimu kutambua kwamba katika kipindi hiki ni muhimu kuwa na fedha ya akiba ili kuweza kuhudumia mahitaji ya familia. Hivyo tahadhari zote za kiuchumi inabidi zichukuliwe ili kuhakikisha kwamba hupati shida katika kipindi hiki kigumu.

Kutoa elimu au kozi mbalimbali kwa njia ya video au mitandao ya kijamii
Ikiwa una ujuzi au utaalamu juu ya kitu fulani basi usikate tamaa, kipindi hiki cha karantini unaweza kuendelea kutoa elimu kwa kupitia mitandao ya kijamii na hata baadhi ya mada kuwafikia watu wengi zaidi kuliko kipindi kingine chochcote kwani watu wako huru na wana muda wa kutosha kusoma na kujifunza zaidi kwa kupitia mitandao hii ya kijamii.

Kununua Hisa
Baadhi ya makampuni ya biashara yanaendelea kufanya vizuri katika masoko yake kutoka na utengenezaji bora wa bidhaa na huduma zingine zitolewazo. Makampuni haya yanauza hisa na ikiwa una akiba ya kutosha ni muhimu kuwekeza katika kununua hisa ili kuendelea kupata faida ambayo itakusaidia kuinuka kiuchumi baada ya karantini ya COVID19 kuisha.

Kufanya kazi za muda wa kujitegemea (freelancing)
Hizi ni kazi ambazo mtu fulani hufanya kwa muda wake aliojipangia na baada ya kumaliza hupata ujira wake hivyo anaweza kuendelea au akaacha baada ya malipo. Mtu mmoja huweza kujifanya kazi mbalimbali kwa kujipangia muda wake mwenyewe. Njia hii huweza kuingiza kipato kikubwa kwa muda mfupi. Baadhi ya programu tumizi (application) kama Freelancer na zinginezo ni nzuri kwa kazi hizi kwa kipindi kama hiki.



Sura ya Tatu

MAHUSIANO
Mahusianona wengine ni jambo la kwanza kwa kiumbe chochote. Hii ni zawadi kubwa ya Mungu toka kuumbwa kwetu. Mahusiano baina ya watu ni jambo la msingi ambalo linatakiwa kuendelezwa katika kipindi hiki kigumu cha karantini.

Katika kipindi hiki, Mahusiano yanaweza kujengwa na kuwa mahusiano thabiti na imara au yanaweza kuharibika kwa sababu mbalimbali. Mahusiano yanajengwa na ukaribu wa watu katika muda fulani. Watu wengi huwa na mahusiano mazuri kwa sababu wanaonana mara kwa mara na hivyo huwasiliani kwa ukaribu. Lakini katika kipindi hiki, watu hawaonani na hivyo hupunguza mawasiliano na hata mahusiano yao hulegea.

Baadhi ya mahusiona yalijengwa kwa sababu watu wanaonana mara kwa mara na hivyo katika kipindi hiki mahusiano yao yako katika kipimo ili kujua uimara wake. Katika kipindi hiki, watu wengi wanakuwa huru na hawajabanwa na majukumu yao ya kila siku kama katika kipindi kabla ya katazo la mikusanyiko ana kuchangamana hivyo ni kipindi kizuri zaidi cha kujenga mahusiano na wenzi wao, watoto, familia na hata ndugu na marafiki wengine kwani hakuna mtu mwenye majukumu mengi sana yanayowafanya kukosa muda wa kuzungumzia mambo yao ya msingi. Zifuatazo ni namna za kujenga mahusiano na watu wengine katika kipindi hiki;

a)       Matumizi sahihi ya muda na watu tunaowapenda
Kipindi hiki cha karantini, watu wengi hawatokina kwenda shemu za mabali na makazi yao hivyo hupata muda mwingi wa kuzungumza na watu wanaowapenda hasa watu wa familia yao kama wazazi, kaka na dada, wenzi wetu, watoto wetu, ndugu, jamaa na marafiki. Kabla ya katazo la kutembea nje au mbali na makazi yetru, watu wengi walikosa muda wa kuzungumza na watu tunaowapenda hivyo katika kipindi hiki tunamuda wa kutosha ili kuzungumza na kuyajenga mahusiano yetu.
b)        Kuzungumza kwa kupitia vyombo vya mawasiliano kama simu, Kompyuta (tarakirishi)
Katika kipindi hiki cha zuio la mikusanyiko na kutotoka nje, tunaweza kuendelea kujenga, kuimarisha na kuendeleza mawasiliano na watu wetu wa karibu kwa kutumia simu au tarakirishi kutumiana ujumbe wa maandishi (meseji na barua pepe) au hata ujumbe wa sauti na hivyo kuendeleza maisha yetu na mahusiano na watu wengine.

c)        Kuzungumza kwa njia ya video
Katika kipindi hiki tunaweza kuendelea na mahusiano yetu na ndugu, jamaa na hata marafiki kwa kutumia mawasiliano ya video. Mitandao mbalimbali ya kijamii kama Instagram, Skype, Viber, FaceBook, WhatsApp, WeChat, SnapChat, Telegram,MySpace, Tumblr, Twitter, Qzone, zoom  na mingine mingi hutoa huduma ya mawasiliano kwa njia ya video maarufu kama Video Chat au Video Conference.

Njia hizi na nyingine nyingi zinaweza kutumika katika kuimarisha mahusiano na watu tunaowapenda na hata kuanzisha mahusiano mapya na watu wengine ili kubadirishana uzoefu katika shughuli mbalimbali na nyanja mbalimbali za maisha.




Sura ya Nne

ELIMU NA MAARIFA
 Karantini ni kipindi ambacho watu wanapata muda ,mwingi kufanya shughuli zaqo nyingi ambazo walikosa kuzifanya kwa usahihi au hawakuweza kuzifanya kabisa kutokana na kutingwa na majukumu mengine. Hivyo katika kipindi hiki, matumizi mazuri ya muda yanaweza kuwa na manufaa makubwa ikiwa tutaishi kwa malengo yakinifu.
 Katika kipindi hiki ambacho shule, vyuo na maktaba mbalimbali zimefungwa ni kipindi ambacho tunaweza kujifunza maarifa tuliyokuwa tunatamani kuyapat kutokana na kuweli kwamba tuna muda mwingi sana wa kuyafanya hayo. Hiki ni kipindi ambacho tunatakiwa kusoma baadhi ya vitabu tunavyovitamani kuvisoma, kurudia vitu ambavyo hatukuvielewa vizuri tukiwa darasani na tukajifunza zaidi kwa kutulia ili kuvielewa.
Karantini inakupa nafasi kubwa zaidi ya kujifunza vitu mbalimbali ambavyo huweza kuwa msaada kwa maisha yako binafsi na hata kwa jamii inayokuzunguka. Kusoma vitabu, kutazama tamthilia, kujifunza maarifa kama kuchora, kupamba, kuandika, kutengeneza programu tumizi, kuandika vitabu au  makala, kuandaa na kufundisha kozi fulani kwa njia ya mitandao, Kuchonga vitu na vingine vingi tunaweza kujifunza namna ya kuvifanya katika kipindi hiki muhimu. Zifuatazo ni njia za kupata na kutoa elimu aua maaraifa fulani:

a)       Kusoma vitabu, tafiti na makala mbalimbali
Karibu ya asilimia 99.99% ya kila kitu hapa duniani kimeandikwa katika vitabu na makala mbalimbali kwa kutumia tafiti au uelewa wa watu fulani juu ya jambo au kitu fulani. Hivyo ili kujifunza zaidi katika kitu fulani tunachokitamani ni muhimu kusoma vitabu, makala na tafito mbalimbali ili kupata ujuzi stahiki juu ya vitu hivyo.

b)       Kuwauliza watu wenye ujuzi wa kitu fulani
Kipindi hiki cha zuio la makusanyiko na kutembea bila sababu za msingi, kinaweza kutumiwa kujifunza ikiwa tutawauliza watu fulani wenye ujuzi juu ya mambo fulanai tunayotaka kuyajua. Tunaweza kuwauliza kwa kutumia barua pepe, mitandao ya kijamii, vikao vya video, ujumbe mfupi au hata kwa kuwapigia simu na njia ya ujumbe wa sauti.

c)        Kutazama video katika mitandao ya kijamii kama Instagram, FaceBook na YouTube.
 Watu wengi hutoa elimu na wengine hujifunza kwa kutazama video mbalimbali na kupata maarifa wayatakayo kwa kutumia njia hii ya mitandao ya kijamii. Waandaaji wa video hizi hufanya hivyo ili kutoa elimu kwa jamii na hivyo ukihitaji elimu hii unapaswa kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili ujifunze mambo mengi mbalimbali.

Njia hizi na nyinginezo nyingi zinawezaa kutumika na hivyo baada ya kipindi cha karantini uinaweza kuwa mtu mwenye mafanikio zaidi kuliko ulivyo leo.

Ninakutakia mapumziko mema na hakikisha unachukua hatua stahiki ili kujilinda na COVID19. Kumbuka; COVID19 inazuilika, jilinde na walinde watu wote wa karibu yako.
Ahsante.




David Duncan Kipeta
Instagram:davidduncankipeta
FaceBook: David Kipeta
+255 659711891(WhatsApp)
+255 753 736983



0 maoni:

Chapisha Maoni